BATUL AFFAR ISMAIL NA WENZAKE
CHAWAKAMA-SUZA
MAKALA
KUHUSU KUIMARIKA NA KUFA KWA JANDO,
UNYANGO NA MICHEZO YA WATOTO ZANZIBAR KAMA NI SANAA YA MAONYESHO
1.0 Utangulizi
•
Asili ya jando
na unyago
•
Maana ya Sanaa
za maonyesho
•
Maana ya Jando
na Unyago
•
Sababu za kuitwa Jando na Unyago
•
Lengo la Unyago
na Jando
•
kuimarika na
kufa kwa jando na unyago.
•
Maana ya michezo
ya watoto
•
Mafunzo ya michezo ya watoto
•
Kuimarika na
kufa kwa michezo ya watoto
•
Dosari
•
Mapendekezo
2.0 Asili ya jando na unyago
Kwa
mujibu wa bwana Mvita Kassim mwanajamii wa mjini Zanzibar ambaye tulifanya nae
mahojiano ya ana kwa ana alisema kwamba
jando Zanzibar linatokana na mila na desturi za uislamu ambazo
zinamtaka muislamu apate sunna na lazima afate utaratibu huo.
Asili ya jando ni nchini Lamu limekuja kutokana na maingiliano ya watu kutoka
Lamu kuja Zanzibar kwa shughuli za kibiashara na misafara ya kidini. Watoto
walikuwa wanafanyiwa jando wakiwa na umri wa miaka 8– 15 hapo hupewa mafunzo
maalum ambayo huzingatia anachoelezwa. Na shughuli ya kutahiriwa hufanywa
alfajiri kando ya mji na hualikwa mangariba wa kila upande kuhudhuriya shughuli
ya jando ili kuepusha mambo ya kishirikina ambayo hufanyika wakati wa
kutahiriwa. Pia huwekwa migomba kwa ajili ya kukabidhiwa wale wazee ambao kwa
bahati mbaya watoto wao walifariki katika zowezi la tohara.
Wari
wakimaliza kutahiriwa hupakwa “Iodine” aidini na hupewa maji ya madafu wanywe
ili wapate kukojowa sana na kidonda kipowe haraka. Pia bwana Mvita alisema
katika mwambao wa pwani zikimalizika shughuli za jando na unyago hakuna
mawasiliano kati ya mangariba na manyakanga kwa kuwakutanisha wari wa kike na
wakiume kwa ajili ya kufanya kwa vitendo
yale mafunzo waliyofundishwa unyagoni au jandoni. Aidha alisema kwamba kuna
tofauti kubwa ya vijana waliopata mafunzo ya jando na wasiopata mafunzo ya
jando. Waliopata mafunzo huwa wanakatazwa kufanya tendo la ndowa kabla ya kuowa
pia kijana akitahiriwa mdogo sana kama miezi miwili au siku arubaini anapofika
miaka 20 nguvu za kiume zinapungua tofauti na alietahiriwa akiwa na umri wa
miaka 8 au 15 au zaidi ya hapo.
2.0.1 Sababu za kuitwa jando
Ni
hiyo silabi ya mwanzo isemayo ja kwa maana ya ukubwa. Na kutowa methali isemayo
“ukubwa ni jaa”. Ja hiyo
imeshabihiana na jando kimaana.
Na
kwa mujibu wa bwana Rashid na Bi Fatma wa mjini Fuoni wanasema kwamba katika
miaka ya 60 vijana walifanyiwa tohara kati ya miaka 14 -20 miaka hii walikuwa
wakipewa mafunzo ya ndowa. Katika miaka ya 70 watoto wa kiume walifanyiwa
tohara wakiwa na umri wa miaka 12 –
16 hapa walifanyiwa sherehe na kupewa mafunzo ya ukakamavu. Katika miaka ya 80
watoto wa kiume walifanyiwa tohara wakiwa namiaka 5 -12 walifanyiwa sherehe tu.
Na kuanzia miaka ya 90 mpaka kuendelea walifanyiwa tohara kuanzia siku 21 au
miezi mitatu au mwaka mmoja ama miwili katika sehemu nyingi za mji wa Zanzibar.
2.1 Lengo kuu la vijana kufanyiwa
tohara
·
Lengo kuu
lakufanyiwa tohara watoto wakiwa na umri mkubwa wenyewe wanasema kwamba ni
kuoneshwa machungu ya kuona kuwa uume si
kitu cha masihara ukautia kwa mwanamke yeyote tu bali asubirie wakati muafaka
wa ndowa yake hali hii ilipelekea
kupungua kwa ngono uzembe.
·
Kumtayarisha
kijana kushiriki katika mambo ya kuongoza jamii yake hususan hiyo ambayo
atakwenda kuanza nayo maisha ya uwili.
2.2. 0 Asili ya unyago Zanzibar
Kwa
mujibu wa bwana Kassim unyago Zanzibar
asili yake kutoka kwa Wangindo wanaoishi
kusini mwa Tanzania na Wamanyema kutoka
Kigoma .Waarabu wa Zanzibar walipendezwa na mila hizo wakawa na ukaribu
sana na watu wa jamii hizo mpaka kupelekea kuowa katika jamii za Wangindo na
Wamanyema ili kufaidika na hayo mafunzo ya jadi.
2.2.1 Sababu ya kuitwa unyago
Ni
manyago yanayofanyika kipindi cha wari kuwekwa ndani na wameita unyago
kwasababu ndani ya unyago kuna vitisho, vitimbwi na mambo ya kinyama ambayo
wanafanyiwa wari hao huwezi kuvielezea vyote ni siri ambazo hazitakiwi kutolewa
nje. Mfano mwari anapelekwa ndani ya chumba chenye giza akisha lizoweya hilo
giza anakuja mtu na koroboi anamwambia aangalie chumba kina nini mwari
anakutana na mtu alielazwa chali kwenye kitanda cha kamba kapakwa rangi usoni
na mwilini kisha katiwa na donge gumu la ladu mdomoni anaambiwa mtu yule
amekufa fanya mizungu yako afufuke kisha anaachwa peke yake.
Pia
hunyolewa nywele za siri kwa kupakwa jivu na kuvutwa nywele hizo kwa mkufu hawatumii
kiwembe. Vilevile hulazwa mwanamke chali na kuambiwa wampandie juu na wakate
viuno mpaka vikatike sawasawa. Hupewa mtu amsugue kwa pumba za mahindi au unga
wakarafuu kama ni somo la kumsuguwa bwana huko aendako. Mambo yote
anayofundishwa huko huambiwa ndio mambo atakayokutana nayo lakini hapo hupewa
somo la usugu wa shida, vitisho, vituko na vitimbwi atakavyovipata kwa mumewe.
Anasulubiwa kusudi apate kuizoweya hali hiyo ya mateso na anatakiwa astahamili
sana .
Kwa
mujibu wa Bi Fatma Juma wa mjini Zanzibar anasema sehemu mashuhuri za kufanyika
jando na unyago ni mwembetanga, kisimamajongoo, kikwajuni na kwahani na kwa
upande wa Pemba ambapo bado shughuli hizi zinafanyika ni kojani, micheweni na
msuka. Na watu mashuhuri waliokuwa wakitajika kwa kufanya shughuli za unyago ni
Bi fatma binti Baraka na Bi Kiboga kwa Zanzibar. Pia alifafanuwa kuwa
mwanachama wa unyago kama anataka mtoto wake afanyiwe unyago anawaalika
manyakanga wote lakini ndani yake anakuwepo nyakanga mkuu wa shughuli hiyo na
nyakanga mkuu ndio anaetowa taarifa za kufanyika kwa unyago. Pia Bi Fatma
alisema wakati wa kufanywa unyago ni magharibi na kama ni wari ambao
hawakufikia muda wa kuolewa hukaa ndani kwa siku saba za ada ambazo mwari huvunja
ungo. Siku ya saba mwari akipelekwa kwao hupambwa kwa kuvishwa nguo mpya na
kusukwa minyosho. Na kama mwari kafikia umri wa kuolewa huwekwa ndani wiki
mbili au miezi mitatu. Mwari huvishwa
kaniki sehemu ndogo tu ya kusitiri uchi wake. Mwari huimbiwa nyimbo kama hii
“
Nifungulie mlango nipite wee
Nifungulile
wee nipite mimi”
Mwari
huenda kufungua mlango kwa magoti na anatakiwa azungumze kwa ishara tu. Nyakanga
humkabidhi mwari kikombe cha liwa ndio salamu yenyewe. Vilevile hakuna
mawasiliano baina ya nyakanga na wari nyakanga kazi yake kutowa mafunzo tu na
si kitu chengine. Inakuwepo na ngoma ya unyago ambayo manyakanga wasaidizi kazi
yao kutoa nyimbo za mafunzo tu. Mfano
wa nyimbo ya unyago anayoimbiwa mwari.
“kanipe
kanipe
Ulipokiweka
kanipe
Kijaluba
cha mwari kanipe
Tena
pelekapeka kwa wakubwa wakarore”
Katika
nyimbo hii mwari huambiwa akachukuwe ushanga uliowekwa kwenye kibao, ushanga
huo huwa umezongwa kama jongoo aliyejikunja. Mwari huamrishwa akauchukue
ushanga huo na aunyanyuwe kwa matako yake kisha akawakabidhi manyakanga wakuu. Na akishindwa kuunyanyua ushanga kwa matako
huimbiwa wimbo huu
“
Msungo kungwi we msungo
Mwari
msungo we mwari
Kungwi
alomtia mwari kitororo
Mwari
wa nyakanga kitororo”
Kwa
kumaanisha kungwi na mwari wake wote wasungo. Ili asalimike kungwi inampasa
akauchukuwe yeye kwa matako aupeleke kwa nyakanga la sivyo mwari atapigwa
shanga za kiuno mpaka kungwi aufikishe na mwari anaona ushanga unavyonyanyuliwa
kwa matako.
2.3 Lengo la unyago kwa vijana wa
kike.
·
Kujenga moyo wa
ujasiri kwa kufuata yale yote anayoelekezwa kwa kutii amri.
·
Kupata heshima
ya kuzungumza na mkubwa wake na atakapokuwa kwa mumewe.
·
Kutokujibizana
na mkubwa wako
·
Kuwa
mstahamilivu pindipo akipata mume mwenye mateso.
·
Kufundishwa
usugu wa kupambana na matatizo atakayokumbana nayo.
2.4.0 Maana ya sanaa za maonyesho
kwa
mujibu wa Semzaba (1997) anasema kwamba ni uonyeshaji wa maisha kisanaa ambapo
mwonyeshaji na hadhiraa huwepo mahali pamoja na wakati mmoja.
Pia
sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa nne za mchezo, mchezaji,
uwanja wa kuchezea na watazamaji kama vile jando, unyago, kusalia mizimu na
masimulizi ya hadithi. (Balisidya na
Muhando)
2.4.1 Maana ya Jando na unyago
kwa
mujibu wa Muhando na Balisidya (1976) ni
aina mojawapo ya kiada yaani miviga ambayo hufanyika kwa wakati wake
maalum ili kuadhimisha wari wanapobaleghe. Kwa ufupi ni ibada ya mpito kwa kuwa
inasaidia watoto kupitia katika mabadiliko ya hadhi kiishara kutoka kuwa mtoto
ambaye alikuwa akiishi katika vitendo vilivyokiuka taratibu za heshima na kuwa
mtu ambaye sasa anapaswa kuishi katika mazingira ya taratibu za tabiya ya
utulivu kwa jamii na kuzifuata.
Kwahiyo
unyago ni mfumo wa elimu isiyo rasmi inayotolewa na makungwi au nyakanga na
ngariba kwa vijana ambao wanatoka katika umri wa utoto na kuingia katika utu
uzima. Hapa hupata mafunzo yanayohusu stadi za maisha na jinsi ya kuishi na
wenza wao.
Na
jando ni kipindi cha mageuzi au mabadiliko ya mtoto kuwa mtu mzima ambaye
anaweza kushiriki katika maongozi ya jamii yake. Jando hili linahusu watoto wa
kiume wasiopungua umri wa miaka 15.
2.4.2 Msimu wa unyago na jando
Unyago
na jando hufanyika wakati wa msimu wa mavuno na vyakula wanavyokula ni vya
kawaida ambavyo huwa wanakula kila siku majumbani kwao pamoja na vinywaji kama pombe ya mtama na togwa. Nyimbo
huwa ni michepuko na kusherehesha shughuli ya unyago na jando. Walioko nje
wasisikie kinachosemwa ndani wala kusikia sauti za wari.
2.4.3. Masharti ya unyago
Masharti
ya unyagoni kwamba kilichofanyika ndani hakiruhusiwi kutoka nje. Na ni mwiko
kumhadithia mtu kilichofanyika ndani ya unyago au mambo uliyoelezwa ulipokuwa
unyagoni.
2.4.4. Mazingira ya unyago na jando
Jando na unyago
hufanyika porini au sehemu iliyo nje ya mji.
2.5 kuimarika kwa jando na unyago
Kwa
mujibu wa Mvungi (1976) ametaja mambo matatu ambayo hufanyika katika jando nayo
ni
·
Kumtahiri kijana
kusimamia uishara wa kifo cha utoto wake.
• Mafunzo
juu ya vipengele vya elimu ya utu uzima katika jamii yake kwa ujumla.
• Kutoka
nje baada ya kumaliza mafunzo hupelekwa kuoga na kuvishwa nguo mpya.
kutokana
na maelezo ya Mvungi na Omar jando na unyago yaliimarika kwasababu wazee
walikuwa wanathamini mambo ya mila na utamaduni pia waliamini kuwa watoto
wanapopata mafunzo ya jando na unyago wanakuwa wamekomaa kiakili na kimwili na
kuweza kushiriki katika kuongoza familiya kwa kutowa ushauri na kufanya mambo
mengine yanayohusu familiya.
kwahiyo
unyago na jando yaliimarika kwasababu ya mashirikiano yaliopo baina ya jamii
moja na nyengine. Pia mahitaji ya jamii hayakuwa makubwa sana kwa wakati ule na
walizingatia zaidi mambo ya mila na desturi zake ambayo kwasasa ni mambo
yaliyopita na hayawezi kurudi tena.
2.6 mafunzo ya jando
Omar
na Mvungi (1981) wametaja baadhi ya mafunzo hayo kuwa ni -:
•
kufunzwa
adabu
•
kujuwa umuhimu
wa kazi
•
kuyajuwa maisha ya utu uzima
•
kuishi vyema
•
kumtayarisha kijana kushiriki katika mambo ya
kuongoza jamii
•
kupata mafunzo
ya mwili na akili.
2.7 Kufa kwa Jando na Unyago.
Kufa
kwa unyago na jando ni kwasababu ya haya mambo ya wigo ambayo jamii yameiga
kutoka nchi za magharibi ili kuchukuwa nafasi ya jando na unyago. Mfano singo,
kitchen party nk mambo haya yamezuka ili kufupisha muda wa shughuli za unyago
na jando.Gharama zinatumika ili kuoneshana makarama nani amefanya jambo jipya
katika shughuli yake. Pia sababu nyengine ni kwamba shughuli hizi za jando na
unyago hazikurithishwa kwa vizazi vipya kutokana na kuonekana ni mila za kishezi zilizopitwa
na wakati.
• MAANA
• Michezo ya
watoto
• Mafunzo ya
michezo ya watoto
• Kuimarika na
kufa kwa michezo ya watoto.
3.0 Maana ya michezo ya watoto
Michezo
ya watoto kwa mujibu wa Haji (2006) ni michezo ambayo watoto wanacheza katika
mazingira yao wanayoishi. Watoto hufanya hivyo kutokana na kuiga mambo ambayo
wanayoyaona katika jamii wanayoishi.
Michezo
ya watoto iko mingi sana kama michezo ya kuigiza ya watoto, foliti, kuruka
kamba, dama, kifichoficho, karata, vitendawili, chemshabongo, michezo
inayoambatana na nyimbo kama kinyuli, kachiri, matango manemane nk. Wanapocheza
michezo hii huwasaidia kuimarisha viungo vya mwili kwa kukimbia, hupata
burudani kwa kuimba na kucheza pamoja na kuigiza michezo mbalimbali kama baba
na mama, daktari, askari, pia kupanuwa akili zao katika kujipatia maarifa ya
chemsha bongo na vitendawili.
3.1 kuimarika kwa michezo ya watoto
Michezo
ya watoto iliwafanya kujenga urafiki kwa kukuza uhusiano uliopo baina ya mtoto
na mtoto kutokana na malezi ya pamoja waliokuwa nayo majirani. Pia michezo hiyo iliwapa nafasi watoto wawe
huru katika kujifunza mambo mbalimbali, kupitia michezo yao hujifunza kuogelea,
kuruka kamba, kuimba, kufanya mazoezi ya kukimbia, kucheza mpira nk. Vilevile
ilijenga mashirikiano katika kuongozana cha kufanya ndani ya michezo yao kama
kuwa daktari na kuigiza sehemu ya daktari na mgonjwa au kuigiza sehemu ya baba
na mama kwa kuigiza matendo wanayoyaona majumbani kwao ama kuigiza nafasi ya
mwalimu na mwanafunzi.
Pia kupitia michezo yao huwa wabunifu kila siku zikiendelea hubuni michezo
mbalimbali kama mchezo wa bui, mchezo wa
farasi, nage, mdako, bao, hadifundo, ukuti, kinyuki kipenyapenya, kigurucheche
ambayo huambatana na nyimbo zake. Aidha
kupitia michezo yao watoto huunda mbinu mbalimbali za kuweza kuwasiliana wakati
ukifika wa kucheza michezo yao. Huanza kwa kuimba au kupiga miluzi ama kuitana
majina wanayopeana katika michezo yao
Kwahiyo hizo ndio sababu kuu zilizofanya michezo ya watoto iimarike
kutokana na mambo ambayo watoto walikuwa wakiyafanya na kufaidika nayo
wanapocheza.
3. 2 Mafunzo ya michezo ya watoto
•
Watoto hupanuwa
akili kwa kupata maarifa mapya kupitia michezo yao.
•
Huwa wabunifu
kwa kuigiza maigizo mbalimbali
•
Kwa wale watoto
wenye uzito katika kusema hupata mazoezi ya kujifunza kusema kwa haraka
•
Huwaondolea aibu
katika kusema mbele ya wenziwao na kuwafanya wawe wachangamfu.
3. 3 .0 Kufa kwa Michezo ya watoto
Michezo
ya watoto imekufa kutokana na mabadiliko mbalimbali katika jamii ambayo
yamesababishwa na muingiliano wa tamaduni tafauti katika jamii mbalimbali. mfano elimu, dini, ubakaji
na uibiwaji wa watoto pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
3.3.1 Elimu
Iimechangia
kwa kiasi kikubwa kufa kwa michezo ya watoto kwasababu wanapokuwa maskuli watoto hupata nafasi ya
kucheza ile michezo wanayocheza majumbani kwao pia masomo ya ziada kwa watoto
hasa somo la kiengereza, hesabati na sayansi yamewafanya watoto wasiwe na
nafasi ya kucheza kutokana na kuwa ule muda ambao wao walitakiwa wacheze wao
huwa wanapata masomo ya ziada kwa ajili ya kuongeza maarifa zaidi.
3.3.2 Dini
Mafunzo
wanayopata watoto wanapokuwepo katika madrasa zao. Mara nyingi watoto huwa
wanafundishwa michezo ya kusali na kuepukana na ibilisi kwa kucheza michezo
isiyo na maana. Hutumia muda wao wakucheza kwa kujifunza maulidi, kuhifadhi
qur-ani, kusoma kasida, kusimuliwa visa vya mitume na kufundishwa michezo yenye
maadili mema kwa jamii yao na kuandaliwa kuwa vijana wema.
3.3.3 Ubakaji na uibiwaji wa watoto
Wimbi hili limepelekea kufa kwa michezo ya
watoto kwasababu hakuna mzazi anayetaka mtoto wake akumbwe na kadhiya hiyo.
Kwahiyo kila mzazi anafanya jitihada ili mwanawe asiwe mbali na nyumbani kwao kwa kupoteza muda kucheza ovyo majumbani
kwa watu. Mzee hufanya jitihada za kumnunulia vitabu mwanawe ajisomee nyumbani
au aangalie michezo ya watoto kupitia televisheni au dvd ama aende twisheni kwa
kuongeza maarifa.
3.3.4 Sayansi na teknolojia
Iimeuwa
kabisa michezo ya watoto kwasababu watoto husikiliza vipindi vya hadithi na nyimbo
kupitia redio, hushiriki katika kujibu masuali ya hadithi au kuimba nyimbo
kupitia vipindi vya hewani vya papo kwa
papo. Hupata nafasi ya kushiriki vipindi mbalimbali vya televisheni na redio.
Huangalia michezo ya kuigiza ya watoto wenzao katika stesheni nyengine za
televisheni. Hucheza gemu kupitia kompyuta na kuangalia katuni mbalimbali
kupitia dvd au video, viwanja vya pembea za kufurahishia watoto, vituo bubu vya
kuchezea gemu mbalimbali kwa wale ambao hawana vitu hivyo majumbani mwao pamoja
na sehemu za kuangalia wanyama kama Zala park na Zanzibar park. Maendeleo haya
yamewafanya watoto wasiwe na muda wa kukaa pamoja na watoto wenzao kucheza kama
zamani.
4.0 Dosari
·
Dosari nyingi
zinazojitokeza katika jamii mbalimbali ni
kutokuelewa umuhimu wa utamaduni wa jamii inayohusika
·
.Wazee
kutokuwarithisha watoto wao mambo ya kimila au watoto kuyapuuza kuona ni mila
zilizopitwa na wakati na kudhani kuwa ni
mila za kishenzi. Kufa kwa unyago na jando ni wigo wa kuzuka mambo mapya katika
jamii yaliopelekea kupuuzwa kwa mila hizo.
·
Kukosekana
malezi ya pamoja kila mzazi analea wanawe apendavyo mwenyewe.
·
Kupungua kwa
mashirikiano baina ya jirani na jirani.
·
Michezo ya
watoto imekufa kutokana na maendeleo mbalimbali yaliyozuka katika jamii zetu na
kupelekea kufa kabisa kwa michezo hiyo ingawa imekuja kwa njia ya video, redio
na televisheni pamoja na viwanja vya kufurahishia watoto. Lakini imeondosha ule
ukaribu waliokuwa nao watoto hapo zamani ukilinganisha na sasa.
·
Kukosekana kwa
uaminifu miongoni mwa vijana, watoto na wazee inayopelekea watoto kubakwa ama
kuibiwa.
5.0
Mapendekezo
Tumeona
sababu mbalimbali zilizofanya kuimarika kwa jando na unyago pamoja na michezo
ya watoto ni malezi bora na mashirikiano ya jamii moja kwenda nyengine. Pamoja
na mafunzo na mbinu mbalimbali wazipatazo kupitia shughuli za kimila za jando
na unyago na michezo ya watoto kama sanaa za maonyesho Zanzibar.
·
Ni mapendekezo
kupitia makala hii kuwatafuta wazee mabalimbali wanaojuwa mambo ya unyago na
jando na kuwaelimisha watu umuhimu wake kupitia magazeti, redio pamoja na
televisheni
·
Kuanzisha
vipindi mbalimbali kuhusu mambo ya mila, silka na tamaduni zetu kupitia makongamano.
·
Kuanzishwa somo
la utamaduni wetu kuanzia ngazi za msingi na sekondari
·
.Kutengenezwa
vipindi maalum vinavyowahusu watoto ili wapate kuona watoto wa zamani walikuwa
wanacheza michezo ipi.
·
Watoto
kuelimishwa mafunzo na faida wanazozipata
kupitia michezo yao. Miongoni mwa mafunzo hayo ni stadi za maisha
wanazofunzwa katika michezo yao ya kuigiza ama hadithi za paukwa pakawa.
MAREJEO
Haji,
M. O. (2006). Vipera vya Fasihi Simulizi. Kidato cha 1- 4. Tanzania.
Makame F.. K. ( mahojiano ya ana kwa ana, 3 Aprili
2015)
Mhando, P na
Balisidya (1976). Fasihi na Sanaa Za Maonyesho. Tanzania Publishing House: Dar-es-salaam.
Muhammed, O.S. (2010).Tasnifu; Mchango Wa Nyimbo Za Unyago Katika Kumkomaza Mwari Kinyumba.
Mvungi, T. A. (1976). Fasihi Simulizi; Katika
Sekondari. Taasisi Ya Elimu: Dar-es-salaam.
Rashid A. R. ( mahojiano ya ana kwa ana, 1
Aprili 2015)
Semsaba, E.
(1997). Tamthiliya ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huriya Cha Tanzania: Dar-es-salaam.
Taratibu M. K.( Mahojiano
ya ana kwa ana, tarehe 20 Machi
2015).
.
Kwanza napenda kutoa pongezi kwa waandaji was makala hii, mada nzuri. Lakini hats hivyo, ninapenda kuuliza suala dogo;
JibuFutaJee, walengwa(wasomaji) was makala hii no waswahili pekeyao ndio uliwakusudia?
Kama c hivyo? Back napenda kutoa ushauri kwamba in vyema ukaainisha maana ya baadhi ya misamiati iliyotumika katika makala hii, kwa mfano; kungwi, nyakanga, mwari, dingo. nk. Hii itasaidia kwa wale wageni wanaojifunza kiswahili na utaduni wa waswahili, kuelewa kwa urahisi makala hii watakapo tembelea blog hii, kwani misamiati hii kwao wao c famial.