NAFASI YA JINSIA KATIKA HADITHI FUPIFUPI ZA KISWAHILI
Na Bishara Mohamed Ali
CHAWAKAMA-SUZA
Jinsia ni mahusiano ya kijamii na kiutamaduni yanayozingatia
mgawanyo wa majukumu kwa kuangalia jinsia ya kike au ya kiume.
Hadithi fupifupi ni aina ya kazi ya sanaa ya utanzu wa hadithi
inayotumia lugha iliyoandikwa katika nathari au iliyo katika masimulizi kama haijaandikwa.
(Msokile, 1992:199). Katika hadithi fupifupi za Kiswahili zimeoneshwa jinsia
zote ambazo ni jinsia ya kike na jinsia ya kiume pamoja na dhima zao
mbalimbali. Nitatumia hadithi fupi ya HAMNAZO, JIRANI MWAMINIFU, ULIMI WA DA
MSIMU na MTU NA HAKI YAKE ili kutathmini nafasi ya jinsia ilivyooneshwa
katika hadithi hizo.
Kwa kuanzia na hadithi ya Hamnazo nafasi ya jinsia imeoneshwa kama
ifuatavyo:
Kwanza, mwanamke ameoneshwa kuwa ni mtu mwepesi/rahisi kujiingiza
katika uasharati. Katika hadithi ya Hamnazo mwandishi amemuonesha Mwanahija
kuwa ni mwanamke ambaye aliyetakiwa na wanaume kimapenzi lakini alikuwa mgumu
kujiingiza katika masuala hayo ila baadae alikubali. Mfano wa hayo unaonekana
katika ukurasa wa 43 mwandishi aliposoma “…pale alipojitia ugumu mpaka
alipolainika kwa haja na mahitaji. Na alipojisabilia akawa kinyang’anyiro
katika ulimwengu muuchu unaouza na kununua kila kitu…”
Vilevile katika jamii jinsia ya kike (wanawake) wanapotakiwa na
wanaume kimapenzi, kwanza hukataa lakini baadae hukubali na kujiingiza katika
uasharati.
Pia katika hadithi fupi ya Hamnazo, mwanamke ameoneshwa kama ni mtu
anaependa starehe na ulevi. Mwandishi amemuonesha Mwanahija kuwa anapenda
starehe na ulevi katika uk.13 pale aliposema, “…na bila shaka tafrija ya jana
alifuzu, na kikao cha ulevi kilikuwa raha tupu”. Aidha katika jamii baadhi ya
wanawake wanajiingiza katika ulevi na kupenda starehe.
Kwa kuongezea mwanamke ameoneshwa katika hadithi hii kuwa hufikia
muda hadhi yake aliyokuwanayo wakati wa ujana wake hushuka. Mwanahija
ameoneshwa wakati wa ujana wake alikuwa akitumia vitu vya thamani kama vile poda,
manukato, nakadhalika lakini baada ya muda kumpita alivikosa vitu vya thamani
na akawa na vitu vyenye thamani duni. Ushahidi wa hayo tunaupata katika uk. 43
kwa kusema:
“siku nyengine alikaa yeye mwenyewe akastaajabu kwamba aliwahi
kutumia poda na manukato ya thamani namna ile, na sasa akijitazama alivyo,
kanzu anazovaa, mafuta ya mkokoriko, wanja wa masizi na poda ya chokaa ya
chumba chake. Ilighasi. Iliuma”. Pia katika jamii jinsia ya kike inapokuwa
katika ujana inakuwa na mambo ya thamani lakini inapopitwa na ujana inavikosa
vitu hivyo.
Vilevile jinsia ya kike, katika hadithi ya Hamnazo imeoneshwa ni
watu ambao wana jeuri kwa wenzao. Mwadishi amemuonesha muhusika Mwanahija kuwa
ni jeuri kwa wenzake, akiambiwa kitu hamjibu aliyemwambia wala hasalimii
wenziwe. Ushahidi wa hayo unaonekana katika uk. 44 mwandishi aliposema: “kama
kawaida Mwanahija aliyekuwa na jeuri kwa wenzake, aliubana kimya, akafungua mlango,
akampita mwenzake bila hata kumtajia “kwi”. He hata mamaangu hunitukani?...” Aidha
katika jamii baadhi ya wanawake wanakuwa wajeuri kwa wenzao wanapoambiwa kitu
wananyamaza kimya wala hawawasalimii wenzao.
Kwa upande wa jinsia ya kiume wameoneshwa katika hadithi ya Hamnazo
kuwa ni watu hadaa na wasio aminika. Mwandishi amemuonesha muhusika Kitwana
kuwa ni mwanamme ambae anataka kumfanyia Mwanahija mambo mabaya. Hali hii
imeoneshwa katika ukurasa wa 44 pale Bi Mtumwa alipomwambia Mwanahija, “Basi
bibi kaja bwana hapa na mjo wake haukunikalia sawa, alitaka kukuona,
nikamwambia hupo. Mimi namuona mwaume yule kanikalia vibaya kweli kweli.
Anakitu anataka kukufanya…” Pia baadhi ya wanaume katika jamii wanawahadaa
wanawake kwa kuwambia wanawapenda kumbe wanataka kuwafanyia vitu vibaya.
Aidha katika hadithi ya Hamnazo, mwanamke ameoneshwa ni mtu
anaesahau maovu anayofanyiwa na mwanamme na kuwa mwenye huruma. Hayo
yameoneshwa kupitia muhusika Mwanahija kuwa alikuwa na mpenzi wake Kitwana ambaye
waliachana, lakini baada ya Kitwana
kurudi na kumtaka tena Mwanahija, alikubali kurudiana nae. Hayo yameoneshwa
katika uk. 44 kwa kusema: “Toka alipokuwa akikoga mpaka alipomaliza, aliwaza
juu ya mfululizo wa kibwana nyumbani kwake, baada ya utengano wa muda mrefu.
Mwisho Mwanahija aliamua kwa ushujaa, “kufa ndio mwisho wa mja… Kitwana na
atende apendalo”…akaupura kwa kiasi chake alitoka bila ya kumuaga Bi Mtumwa”.
Vile vile wanawake wengi katika jamii baada ya kufanyiwa maovu na mabwana zao
au waume zao wanakuwa ni wepesi wa kusamehe na kurudiana nao.
Kwa kuendelea na hadithi ya Jiarani Mwaminifu nafasi ya jinsia
imeoneshwa kama ifuatavyo:
Kwa kuanzia na jinsia ya kiume imeoneshwa kwamba wanaume ndio wasimamizi
wakuu wa familia na wanapaswa kuzilinda na kuhakikisha usalama wa familiya zao.
Katika hadithi hii Bwana Saidi alikuwa mkali kwa watoto wake na hakuwaruhusu
kutoka nje na kubwa zaidi katika nyumba yake hakuruhusu mwanamme yoyote
kuingia. Mfano mwandishi anasema katika uk.51 kuwa, “ Bwana Saidi alikuwa baba
mkali. Watoto wake wa kike kabisa hakuwaruhusu kutoka nje na ndani ya nyumba
yake hakumuachia mwanamume yoyote kuingia”. Aidha katika jamii wanaume ndio
wasimamizi wakuu wa familia zao na huzilinda na kuhakikisha usalama wa familia
hizo.
Pia hadithi hii imeonesha jinsia ya kike kwamba wanawake ni watu
ambao hawaaminiki hata uwaone wana imani nzuri ya dini lakini wanafanya mambo
machafu kwa siri ya hali ya juu. Hali hii imejitokeza katika uk. 52 kupitia
muhusika Bi Mtumwa ambaye aliaminika kuwa ni mcha Mungu, yaani mtu mwenye imani
ya dini na kukesha usiku kwa kufanya ibada. Lakini kumbe usiku ule hakuwa
akikesha kwa kufanya ibada isipokuwa alikesha kwa kufanya uovu, yaani alikesha
na mwanamme. Mwandishi ameeleza hivi:
“… watoto walipelekana chooni wakati wa kurudi mmoja ghafla alitupa
jicho nje. Bibi mmoja alikuwa katandika kizulia uwanjani kakaa na kijana wa
kiume. Polepole watoto waliingia chumbani kwao wakazima taa halafu wakanyatia
mpaka kwenye dirisha lao lililokuwa limefungwa wakachungulia kwenye virukia.
Walipotazama vizuri walimuona Bi Mtumwa. Baada ya kujifurahisha kwa muda
walinyemelea wakarudi vitandani mwao”. Aidha katika jamii wapo baadhi ya
wanawake ambao wanaonekana ni wachamungu kumbe ni kinyume chake, huwa wanafanya
maasi kwa kuwa na wanaume ambao hawajawaoa.
Vilevile katika hadithi ya Jirani Mwaminifu jinsia ya kike
imeoneshwa ni watu wanaoishi vizuri na majirani zao na kuwa tayari kusaidiana pindi
mmoja akipatwa na matatizo. Haya yameoneshwa kupitia muhusika Bi Mtumwa
alipokubali kwenda kukaa na watoto wa Bwana Saidi siku ile ambayo walifiliwa na
iliwabidi waende shamba katika msiba yeye na mkewe. Ushahidi wa haya umeoneshwa
katika uk.52 mwandisi aliposema, “usiku ulipoingia Bi Mtumwa alifika. “sasa
watoto tukishakunywa chai mwende zenu kupumzika”. Pia katika jamii wako baadhi
ya majirani ambao wanaishi vizuri na wanaelewana , vilevile wako tayari
kusaidiana pindi mmoja anapofikwa na tatizo.
Kwa upande wa hadithi fupi ya Ulimi wa Da Msimu imeonesha nafasi ya
jinsia ya kike na ya kiume kama ifuatavyo:
Kwa kuanzia na jinsia ya kiume, mwandishi ameionesha jinsia ya
kiume kuwa ni watu wanaotumia mamlaka yao vibaya kwa kuwatawisha wake zao ndani
bila ya kutoka nje wakati wanapoondoka. Hali hii inaonekana kupitia Machano
ambaye aliondoka kwenda shamba na kurudi baada ya siku mbili, hivyo alimwambia
mkewe ambaye ni Ashura asitoke akiwa yeye hayupo. Mwandishi ameionesha hali hii
katika ukurasa wa 79 pale Machano aliopomwambia mkewe, “mimi ninakwenda shamba
nitarudi kesho kutwa nikijaaliwa. Lakini sitaki utoke nikiwa sipo”. Aidha
katika jamii wapo baadhi ya wanaume wanaotumia mamlaka yao vibaya kwa
kuwatawisha wake zao wasitoke nje pindi wakiondoka.
Aidha jinsia ya kike imeoneshwa kuwa ni watu wakarimu. Ukarimu
unaonekana kupiti Ashura ambaye alimsisitiza mumewe aende na zawadi shamba, pia
alimkirimu chai na uji jirani yake ambaye ni Da Msimu baada ya kwenda nyumbani
kwake. Haya yameoneshwa katika ukurasa wa 79 Ashura aliposema:
“Nenda na kizawadi urudi na kipakacha”.
“… karibu Da Msimu…
chai,uji, karibu hiyo”.
“vyote vipo usitie wasiwasi”.
Pia jinsia ya kike katika jamii wanakuwa ni watu wakarimu kwa
wageni wao na kuwahimiza waume zao wanapoondoka wachukue zawadi ili wawapelekee
wanakokwenda.
Pia katika hadithi ya Ulimi wa Da Msimu imeoneshwa jinsia ya kike
ni watu washawishi na wafitinishaji wa ndoa za wenzao na kuwa wasaliti. Hayo
yameoneshwa kupitia muhusika Da Msimu ambaye alimshawishi Ashura aende katika
beni bila ya ruhusa ya mumewe na kumshawishi alewe. Ashura alifanya kama
alivyoambiwa na Da Msimu. Hayo yanaonekana katika ukurasa wa 80-82 kwa kusema:
“kwanza atajuaje kama umekwenda?” Msimu alimwambia Ashura… sura
mbilimbili babu we, utamwambia alikuwa mtu mwengine huyo.” Lakini baadae
alipata matatizo ya kuumia mguu na kuchunika uso. Baada ya kupatwa na matatizo
hayo Da Msimu alimgeuka Ashura na kumwambua atajijua na mumewe. Pale aliposema,
“ mtu akiambiwa na yeye hujiambia ati, ukiambiwa twende utakwenda tu, au fanya
utafanya tu? Atatambuana mwenyewe na mumewe”. Vile vile katika jamii wanawake
wanaonekana kuwa ni washawishi , wafitinishaji wa ndoa za wenzao na huwasaliti
baada ya wenzao kupatwa na matatizo.
Vilevile hadithi hii imeonesha jinsia ya kike ni yenye kupinga amri
za waume zao. Hali hii tumeiona kupitia Ashura ambaye aliamua kwenda katika
beni ingawa aliambiwa asitoke nje na mumewe wakati akiondoka. Mwandishi ameionesha
hali hiyo katika ukurasa wa 80 kwa kusema:
“Ashura alikuwa katikati kazongwa haonekani, kachukuliwa kabisa na
ngoma hasikii haoni…”
Pia katika jamii wapo wanawake ambao wanapinga amri za waume zao
wanapoambiwa wasitoke nje ikiwa waume zao hawapo, lakini huwa wanatoka nje na
kwenda wanakopenda.
Kwa kumalizia na hadithi fupi ya Mtu na haki yake nafasi ya jinsia
imeoneshwa hivi:
Kwanza jinsia ya kiume imeoneshwa kuwa ni wafanyabiashara. Katika
hadithi fupi ya Mtu na haki yake imeoneshwa jinsia ya kiume kuwa ni
wafanyabiashara kupitia kijana aliyekuwa anauza kofia ya viua vya lasi. Mwandishi
amemuonesha kijana huyo katika ukurasa wa 25 aliposema:
“Khamis alipomwona kijana mmoja anazabuni kofia ya viua vya lasi
njiani na yeye alisimama.
“Je, biashara hiyo?”aliuliza.
“Ndio”, alijibu mwenye kofia…”
Aidha katika jamii jinsia ya kiume inajishughulisha zaidi katika
kufanya biashara ya kurandisha vitu (bidhaa) mitaani kuliko jinsia ya kike.
Kwa kuongezea, jinsia ya kiume imeoneshwa kwamba ni watu matapeli. Katika
hadithi ya Mtu na haki yake wanaume wameoneshwa kuwa ni matapeli. Kupitia
Khamis ambaye alitaka kumtapeli muuza kofia kwa kuichukuwa kofia yake na hakuwa
na lengo la kumlipa. Khamis ameoneshwa katika uk. 25-26 utapeli aliokuwa
anataka kumfanyia muuza kofia kwa kusema: “Khamis hajawa na mpango maalumu:
alibaki kutegemea bahati tu. Alikuwa na tamaa kwamba labda anaweza kufanya njia
hata atokee kwa mlango wa nyuma wa Chuo na kupotelea mbali”. Pia katika jamii
jinsia ya kiume kwa kiasi kikubwa ndio wanaoongoza kwa kutapeli wenzao katika
biashara.
Vilevile, jinsia ya kike imeoneshwa kuwa ni waalimu wa Chuoni
(Madrasa). Katika hadithi hii mwanamke ameoneshwa ni mwalimu wa Chuo cha
Qur-ani katika ukurasa wa 26 ambapo mwandishi amesema:
“Bi Mwalimu nina mwanangu nataka kumtia Chuoni, “ Khamis alimwambia
Bi Mwalimu baada ya kumuamkia kwa adabu”. Aidha wapo wanawake katika jamii
ambao ni waalimu wanaosomesha katika vyuo vya Qur-ani (Madrasa).
Pia katika hadithi ya Mtu na haki yake jinsia ya kiume imeoneshwa
ni wafanya kazi wa serikali katika Wizara ya Ulinzi (Askari). Wanaume katika hadithi
hii wameoneshwa kuwa ni askari ambapo miongoni mwa kazi zao ni kuwakamata wanaodhulumu
wenzao. Kwa hivyo Khamis baada ya kuona askari alifadhaika kutokana na utapeli
ambao alikuwa anataka kuufanya. Haya yameoneshwa katika ukurasa wa 26 mwandishi
aliposema:
“kutupa jicho nje aliona askari wawili wanasogelea upande wa Chuoni:
ubabaifu na hofu ulichanganyika kumfanya mwehu ghafla”. Vilevile katika jamii
wapo wanaume wanaofanya kazi ya uaskari: Pia kuna baadhi ya watu wanapowaona
askari ikiwa wamefanya kosa wanakuwa na ubabaifu na kuogopa kukamatwa.
Kutokana na maelezo ya hadithi fupifupi nne nilizozitumia ambazo ni
hadithi ya Hamnazo, Jirani Mwaminifu, Ulimi wa Da Msimu na hadithi ya Mtu na
haki yake, hivyo ndivyo jinsi nafasi ya jinsia ilivyooneshwa katika hadithi
fupifupi za Kiswahili.
MAREJEO
M, M. Mulokozi. (1996). Fasihi ya Kiswahili. Tanzania: Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania.
Mohammed, S. A & Ali, A. M. (1981). Hapa na Pale.
Zanzibar: Taasisi ya Kiswahili na Lugha za
Kigeni/Wizara ya Elimu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni