Jumanne, 5 Julai 2016

UCHAWINI KUNA MAMBO
1.      Ukitaka ngia huko, wallahi utashituka
Utakutia vituko, vivyo navyo patashika
Utajutia kuwepo, na huruma kukushika
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

2.      Vizuu wa uchawini, kiwaona tashituka
Tadhani ni hayawani, hali imebadilika
Si kichwa si miguuni, sura zao kama paka
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

3.      Viongozi wa wachawi imeni imewatoka
Yao kwa hustawi, vizuu kupukutika
Ta siku moja haiwi, mmoja akasikika
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

4.   Uchawini ni hatari, ukatili meongoka
Kuna watu majabari, tena wasotikisika
Wamekuwa majeuri, kwa kile wanachotaka
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

5.      Ajira ya uchawini,  kama ya mkwe na kaka
Mavunoye huyaoni, ni viboko na kuchoka
Utaona kisirani, na akili kukuruka
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

6.      Ukichoka uchawini, kamwe usijeropoka
Watakuweka pembeni, na njaa itakufika
Ubakie masikini , iwe huna pa kushika
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

7.      Siku ukiwa na ombi, ndipo hapo utachoka
Waonekana cha zombi,  ulokosa pa kushika
Utakuwa cha mbirimbi, kwa kisu utakatika
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

8.      Mwisho naliweka tojo kuonesha nimefika
Uchawini si porojo, kila mtu akacheka
Utanywishwa ta mkojo, watu kimya kukuweka
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

NA: SALEH ZAHRAN ABDULLA- CHAWAKAMA-SUZA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni