Jumatatu, 4 Julai 2016



NAMNA USHAIRI UNNAVYOFANANA NA KUTAFAUTIANA NA NGONJERA

NA:SALEH ZAHRAN----CHAWAKAMA-SUZA
Katika makala hii tutaangalia katika sehemu kuu nne. Kwanza tutaeleza fasili ya Ushairi na Ngonjera kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali. Pia tutaeleza tafauti za ngonjera na ushairi. Vile vile  tutaeleza mfanano wao na mwisho tutamalizia na  hitimisho.
 Kwa kuanzia na  fasili mbalimbali:
Kwa mujibu wa  Masebo ( 2001) anasema ushairi ni sanaa inayopambanuliwa  kwa mpangilio maalum wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha au  sitiari au ishara, katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo ili kueleza tukio, wazo au hisi fulani kuhusu maisha au mazingira ya binaadamu, kwa njia inayogusa moyo.
 Pia ushairi ni kazi za fasihi zinazojumuisha matumizi ya mapigo ya kimuziki. (Kaduguda na wenzake 2009).
Kiujumla tunasema kuwa ushairi ni tanzu ya fasihi ambayo hutumia lugha nzito, ya mkato, matumizi ya lahaja, fasaha ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa ambapo kwa upande wa ngonjera ni kai ya fasihi ambayo hutumiya lugha tafauti na ushairi.
Ngonjera kwa mujibu wa BAKIZA (2010) ni ushairi unaotambwa kwa njia ya maigizo ya majibizano.
Vilevile ngonjera ni mashairi ya kujibizana baina ya watu wawili au zaidi. (Mvungi, 2010).Kwa ujumla ushairi na ngonjera unaonekana kutafautiana sana na hii ni kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo:-
Ushairi  ni kati ya tanzu kuu nne za fasihi simulizi ambazo ni ushairi, semi, maigizo na hadithi  ilihali ngonjera ni kati ya kipera cha ushairi chenyewe ambacho ni mashairi, tenzi, nyimbo, maghani na ngonjera.
Ushairi unakuwa na wazo moja linaloelezea juu ya jambo fulani wakati ngonjera huwa ni wazo moja lenye majibizano bila ya kuwepo majibizano haitokuwa ngonjera.
Halikadhalika ushairi una vipera vingi kama vile ngonjera, maghani, tenzi, tumbuizo lakini ngonjera haina vipera ndani yake chenyewe ni kipera cha ushairi.
Pamoja na hayo ushairi huweza kughaniwa na muhusika mmoja wakati ngonjera hutambwa au kuigizwa kuanzia wahusika wawili na kuendelea.
Vilevile ushairi hufuata kanuni zote za kimapokeo, kimamboleo pamoja na kimajaribio lakini ngonjera hufuata kanuni ya kimapokeo tu. Mfano beti, vina, mizani, urari, kibwagizo, muwala nk huwa ni sawa kama vile zilivyo kwenye mashairi ya kimapokeo tu.
Pia majibu au  suluhisho la ushairi hutolewa na mhakiki anayeisoma kazi hiyo ya ushairi lakini ngonjera suluhisho lake hutolewa na watambaji wenyewe au mtunzi aliyetunga kazi hiyo mwisho wa ngonjera yenyewe.
Ushairi hutumia lugha ya mafumbo na lugha ya mkato  lakini ngonjera hutumia lugha nyepesi na sanifu ambayo msikilizaji au mtazamaji huweza kufahamu kwa urahisi zaidi.
Mfano wa shairi ambalo limetumia lugha ya mkato. Lugha hii imeweza kutowa ujumbe uliokusudiwa. Katika kitabu cha Kimbunga uk: 12.
                                          RUSHWA
                           Rushwa kajenga kambi,       na kuondoka hataki
                          Afanya kila vitimbi,             mkaidi hashindiki
                          Tumzushieni wimbi,             isiwe kutuhiliki
                           Tumchimbie handaki,            rushwa tukamzikeni.
Mfano wa ngonjera ambayo haiwezi kutumia lugha ya mkato kutokana na muundo wake. Katika kitabu cha Kiswahili kwa Shule za Sekondari Kidato cha 2 uk: 111
CHUMA:            
Ndugu tega sikio,              maoni kutekeleza,
                         Mwisho nipe itikio,           kwayo niliyoeleza
                         Pasiwepo singizio,             au yangu kuyabeza,
                         Rushwa ndani ya haki,       haifai kutumia.
SHOMVI:      
Nakuona wajivunga,                  hunalo la maana,
                    Na kamwe hayana mwanga,      nieleweni bayana,
                    Kaa njaa ukiganga,                     ukidhani rushwa lana,
                    Bila kupokea rushwa,                 tumbo haliwezi shiba.
Ushairi hauzingatii mambo ya uigizaji katika jukwaa lakini ngonjera inazingatia mambo muhimu ya uigizaji katika jukwaa kama vile maleba, matumizi ya vifaa vya uigizaji pamoja na vitendo vya wahusika jukwaani.
Ushairi unaweza kuwa na idadi nyingi  au idadi chache ya beti ( beti moja) na kuweza kutosheleza kinachozungumzwa lakini ngonjera haiwezi kuwa na idadi chache (beti moja)  na kuweza kujitosheleza. Mfano shairi la Rushwa uk: 12 katika kitabu cha Kimbunga lina beti moja yenye kujitosheleza na shairi Macho uk: 27 katika kitabu cha Raha Karaha lakini pia shairi la Rushwa katika kitabu cha Kimbunga.


Mbali na tafauti hizo zilizojitokeza kati ya usahiri na ngonjera pia kuna mlingano wake nazo ni -:
Ushairi na ngonjera ni tanzu za Fasihi Simulizi ingawa ngonjera haijitegemei kama ulivyo ushairi. 
                            FASIHI SIMULIZI
HADITHI
USHAIRI
SEMI
MAIGIZO

Ngonjera, maghani mashairi, tenzi, nyimbo



Pia zote kwa pamoja hutumia beti na urari wa mizani na vina. Mfano wa  ubeti wa shairi wenye urari wa vina na mizani.
                   Ja/ma/ni/ ni/me/i/cho/ka,          a/dha/ hi/i/ si/i/ta/ki
                    Mnyonge nadhalilika,             nchini sihitajiki
                    Hakuna kinacholika,               nilacho hakisemeki
                    Kwangu tabu na mashaka,      kama uji na mgonjwa.
Mfano wa ubeti wa ngonjera wenye urari wa vina na mizani.
Ado:            Wa/li/mwe/ngu/ na/u/l/iza,         ma/ji/bu/ m/ni/pa/t/ie,
                    Kichwani naona kiza,                utando mnifutie,
                     Acheni kuniburuza,                   maelezo tafutie,
                     Ajira kwao watoto,                    tija gani mnapata?
Vilevile ushairi na ngonjera hughaniwa katika mahadhi tafauti itategemea  na uamuzi wa wanaoghani hiyo ngonjera au ushairi.
Halikadhalika zote kwa pamoja hutowa hisi na tafakuri katika ulimwengu. Mfano hisia na msisimko juu ya  ugonjwa wa Kipindupindu, UKIMWI, Mauaji ya Albino Ajira kwa watoto nk.
Ngonjera na ushairi huwasilishwa jukwaani, katika  kumbi mbalimbali, katika sherehe mbalimbali na kwenye vyombo vya habari.
Aidha zote hutumia ubunifu wa lugha ambao huleta mdundo na msisimko wakati wa kuimbwa, kughaniwa au kuigizwa. Mdundo hupatika katika urari wa vina vilivyotumiwa katika shairi au ngonjera.
Ngonjera na ushairi hutumia mtindo wa masimulizi katika kuonyesha wakati na mandhari iliyotumika.
Mfano wa shairi ambalo limetumia mtindo wa masimulizi ni shairi Kibwangai uk : 9 katika kitabu cha Kimbunga.
             Kuna hadithi ya kale,           kwa babu nimepokeya
             Kwa manyani zama zile,       mkasa ulotokeya
             Nilikuwa mwanakele,            hayo nikazingatia
             Leo nawadokezeya,               kwa nilivyoyafahamu.
Mfano wa ngonjera ambayo imetumia masimulizi ni ngonjera ya Ujamaa Vijijini uk : 107 katika kitabu cha Kiswahili kwa shule za Sekondari kidato cha pili.
Msimulizi
                  “Kijana aliingia,                   ndani kutoka shuleni,
                   Kakuta waongea,                wazaziwe sebuleni,
                   Hima aliamkia,                    na akaketi kitini,
                   Mara mama kwa huzuni,     sauti ikamtoka”
Kutokana na maelezo hayo ngonjera na ushairi zinatafautiana na kulingana kwa kuziweka pamoja katika nyanja za ushairi.  Kwahiyo tunaona ni jinsi gani zilivyotafautiana katika tanzu na vipera,  namna ya uwasilishaji wake, wahusika, katika kanuni zake, utowaji wa suluhisho, matumizi ya lugha, idadi ya beti pamoja na mambo ya kuzingatia wakati wa kuigiza. Halikadhalika shairi na ngonjera hufanana katika utanzu wa fasihi simulizi, urari wa beti wenye kuzingatia mizani na vina, utoshelevu wa beti, hutumika katika mukhtadha maalum, hutumia ubunifu wa lugha wenye kutowa msisimko na mdundo ndani yake, mtindo wa masimulizi pamoja na kutowa hisi na tafakuri.




MAREJEO
BAKIZA (2010). Kamusi la Kiswahili Fasaha.  Oxford University Press.   Dar- es- salaam.
Masebo, J. A na Bukagile, G, R. (2007). KISWAHILI; KWA SHULE ZA SEKONDARI. Kidato cha Pili. Nyambari Nyangwine Publishers: Dar Es Salaam.
Kaduguda, R. Na wenzake ( 2009) Kiswahili Shule za Sekondari, Kidato cha Kwanza.  Oxford University Press: Tanzania.
Mvungi, Th. A. (1982). Raha Karaha. CONTINENTAL PUBLISHER LIMITED:  Dar es salaam.
Haji, G. H. ( 1998). Kimbunga.  Dar es salaam University Press. Dar es salaam.
Mvungi, Th, A ( 2010 ).  Kiswahili Kidato cha 1 na 2. Ben and company Ltd. Dar- es -salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni