Alhamisi, 7 Julai 2016



NA:    HAITHAM  HASSAN OMAR
          SALEH ZAHRAN ABDULLA
          SALUM ABBASS
CHAWAKAMA-SUZA

MAKALA MUHIMU JUU YA ISTILAHI MBALI MBALI ZINAZOTUMIKA KATIKA UFUNDISHAJI  NA MASUALA YA KIELIMU NA UJIFUNZAJI KATIKA LUGHA YA KISWAHILI
Makala hii itakuwa na sehemu mbili ambazo ni fasili mbalmbali za msamiati. Lakini kwa sehemu ya pili itakuwa na MISAMIATI mbalimbali inayotumika katika ufundishai na ujIfunzaji

Kwa kuanzia na fasili ya neno “MSAMIATI ni kama ifuatavyo
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004), Msamiati ni jumla ya maneno katika Lugha.
Kwa mujibu wa Kamusi Teule ya Kiswahili (2014), Msamiati ni maneno yote magumu na rahisi ya Lugha yoyote inayotumika.
Katika sehemu hii tunaonesha misamiati mbalimbali yanayotumika katika ufundishaji na ujifunzaji. Misamiati hiyo ni kwa lugha ya Kiswahili.
Kwa hivyo, misamiati ni maneno yanayotumika katika lugha fulani, mara nyingi hutumika kumaanisha maneno mapya au maneno yasiyojuulikana na watu wengi. Msamiati hutumika kufafanua maana ya maneno yanayopatikana katika muktadha mbali mbali. Mfano msamiati wa skuli, maneno yanayotumika sana katika mazingira hayo hayawezi kutumika kiasi kikubwa katika mazingira mengine kama hospitali. Yafuatayo ni misamiati (50) ya Kiswahili inayotumika katika uwanja wa elimu na ufundishaji:
1.      Upimaji (Assessment): Ni mbinu inayotumika katika kujua mafanikio ya ufundishaji  na ujifunzaji unavyoendelea darasani. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
2.      Jaribio (Test): Ni namna ya upimaji ama kwa njia ya maswali au vitendo ili kupima  kama mada  iliyosomeshwa imefahamika au haikufahamika. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
3.      Muhula (Term): Ni kipindi maalumu kwa ajili ya masomo ambacho tathmini ya jumla ya maendeleo ya masomo yote hufanywa. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
4.      Ripoti (Report): Ni taarifa maalum inayoandaliwa skuli kwa maendeleo ya wanafunzi katika masomo yao. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
5.      Takwimu (Almanac): Ni taarifa za ukweli kuhusu mwanafunzi zinazoonesha maendeleo yake ya kusoma na kujifunza katika kipindi maalum. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
6.      Alama (Marks): Ni alama zinazotolewa na mwalimu kuonesha daraja au kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi katika somo. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
7.      Matokeo (Result): Ni takwimu ya kazi zilizofanywa na mwanafunzi kuonesha namna ya mafanikio na udhaifu wa tendo la kujifunza na kufundisha. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
8.      Dodoso (Questionnaire): Ni zana au mbinu inayotumiwa na mwalimu kupata taarifa za kina (halisi na sahihi) katika tendo zima la ufundishaji na ujifunzaji. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
9.      Chemsha bongo (Quiz): Ni fumbo au mafumbo yenye lengo la kuchokoza udadisi na wepesi wa wanafunzi kujibu au kujiweka tayari na tendo la kujifunza. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
10.  Maendeleo (Progress): Ni tathmini ya mwenendo mzima wa mwanafunzi katika tendo la kujifunza ama kusonga mbele au kurudi nyuma. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
11.  Mahihisho (Corrections): Ni tendo linalotumika kumrekebisha au kumkosoa mwanafunzi ili asiweze kurejea tena kosa hilo na kujua usahihi wake. Msamiati huu ni katika uga wa tathmini.
12.  Tathmini (Evaluation): Ni njia inayotumika kupata taarifa ni kwa kiasi gani malengo ya ufundishaji yamefikiwa kukifuatiliwa na maamuzi muafaka. Msamiati huu ni katika uga wa upimaji.
13.  Uwasilishaji (presentation): Ni msamiati unaotumiwa na mwalimu katika hatua ya kufundisha ili kutoa maarifa mapya au muendelezo wa somo katika tendo la kujifunza. Msamiati huu ni katika uga wa kufundisha.
14.  Viwango (Standard): Ni msamiati unaotumika kutoa maelezo kuhusiana na vipi wanafunzi wanapaswa kufika katika sehemu fulani kwenye matokeo yao. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
15.  Azimio la kazi (scheme of work): Ni buku maalumu la mwalimu linalomuongoza kufundishia mada zilizovunjwavunjwa kutoka katika muhtasari ili zisomesheke kiurahisi katika wiki, mwezi au muhula. Msamiati huu ni katika uga wa Mitaala.
16.  Andalio la somo (lesson plan): Ni buku maalumu la mwalimu linalomuongoza kufundishia mada zilizovunjwavunjwa kutoka katika azimio la kazi ili zisomesheke kiurahisi katika kila kipindi. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
17.  Njia (Methodology): Ni mbinu inayotarajiwa kutumika katika kufanikisha suala zima la upatikanaji wa elimu kwa namna inavyofaa kwa wanafunzi husika. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
18.  Mwendo (Course): Msamiati huu unatumika katika kujumuisha mwenendo mzima wa masomo ambayo wanafunzi wanategemea kujifunza katika kipindi kilichokusudiwa. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
19.  Mafanikio (Achievement): Msamiati huu unatumika katika kuonesha ni kwa jinsi gani wanafunzi wamefanikiwa. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
20.  Rejea (Reference): Msamiati huu hutumika katika kumsaidia mwalimu na mwanafunzi kufanya kazi zao na hata katika kujifunza  na kufundishia pia kuonesha uthibitisho wa kazi mbali mbali mbali za kitaaluma. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
21.  Maudhui (Content): Msamiati huu hutumika katika kuonesha mtiririko mzima wa somo kuanzia mwanzo wa somo hadi mwisho wa somo. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
22.  Ujuzi (Competence): Msamiati huu pia hutumika katika kuonesha  maarifa  aliyoyapata mwanafunzi kutokana na kile alichojifunza baada ya kumaliza somo. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
23.  Marekebisho (Adjustment): Ni msamiati ambao unatumika kuwaeka sawa wanafunzi, walimu na hata watu wa mitaala pale endapo patatokezea kasoro au patajitokeza tatizo lolote katika kazi zao. Msamiati huu ni katika uga wa mitaala.
24.  Kompyuta (Computer): Ni zana au kifaa kinachotumika kutafutia elimu, kuandikia, kuchorea picha na michoro mengine mbali mbali katika tendo zima la kufundisha na kujifunza. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
25.  Maktaba (Library): Ni sehemu ambayo hutumika kwa kujisomea vitabu, majarida, magazeti nakadhalika kwa ajili ya kujiongezea maarifa na ujuzi katika tendo zima la kufundisha na kujifunza. Msamiati huu ni katika uga wa zana za kufundishia.
26.  Mabango (Posters): Ni aina ya zana au kifaa cha kufundishia na kujifunzia ambazo hutumika kuonesha picha na michoro ya vitu mbali mbali ambavyo si rahisi kuvileta darasani wakati wa usomeshaji. Msamiati huu ni katika uga wa zana za kufundishia.
27.  Kamusi (Dictionary): Ni aina ya kitabu ambacho hutumika kujua maana, tahajia, miundo na matamshi ya maneno mbali mbali katika lugha kwa ajili ya kujiengezea taaluma na misamiati. Msamiati huu ni katika uga wa zana za kufundishia.
28.  Runinga (Television): Ni kifaa ambacho hutumika katika kupata maarifa mapya kwa njia ya kuona picha na kusikia taarifa na matukio mbali mbali katika tendo zima la kujifunza kwa kutumia njia za kisasa za sayansi na teknolojia. Msamiati huu ni katika uga wa zana za kufundishia.
29.  Maigizo (Role play): Ni aina ya mbinu za kufundishia ambayo hutumiwa na mwalimu darasani ili kujenga ari na shauku za wanafunzi katika kulipenda somo ili lengo lililokusudiwa lifikiwe. Msamiati huu ni katika uga wa mbinu za kufundishia.
30.  Mjumuisho (Inclusive): Ni ufundishaji unaojumuisha pamoja wanafunzi walemavu na wasio walemavu, unaotumika skuli katika kuondoa ubaguzi na unyanyasaji ili wanafunzi waweze kujifunza kwa kushirikiana na kusaidiana. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
31.  Takriri (Repetition): Ni mbinu ya inayotumiwa wakati wa ufundishaji inayowafanya wanafunzi kurudiarudia neno au sentensi kwa lengo la kutilia mkazo na kujenga kumbukumbu ya kudumu. Msamiati huu ni katika uga wa mbinu za kufundishia.
32.  Ushirikishaji (Participartion): Ni njia ya ushirikishwaji wa wanafunzi katika somo, unaotumika kuwafanya wanafunzi wote wawe na utayari wa kutenda na kujaribu wakati wote  wa tendo la kufundisha  na kujifunza. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
33.  Mazingira/Muktadha (context): Ni mazingira halisi au yakubuni yanayotumiwa ili kuwawezesha wanafunzi kujenga ufahamu wa mada kwa urahsi zaidi pamoja na kumsaidia mwalimu kufahamika ipasavyo katika ufundishaji wake. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
34.  Ubunifu (Creations): Ni uwezo wa kutenda mambo mbali mbali unatumiwa na mwalimu na wanafunzi katika kuonesha ustadi na umahiri wao katika tendo zima la kufundisha na kujifunza. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
35.  Wakufunzi (Trainers): Ni wataalamu walioteuliwa kwa lengo la kutoa mafunzo ya aina mbali mbali kwa walimu (TRAINERS) ambayo yatatumika kuboresha uwezo wao katika utendaji na kupelekea mabadiliko katika utendaji wao wa kazi. Msamiati huu ni katika uga wa mafunzo.
36.  Kinasa sauti (Tape recorder): Ni aina ya kifaa ambacho hutumika kuwapa wanafunzi ujuzi wa kusikiliza maneno, hadithi na habari mbali mbali kwa ajili ya kufanya uchunguzi na uchanganuzi wa kile walichokisikia. Msamiati huu ni katika uga wa zana za kufundishia.
37.  Mrejesho (Feedback): Ni taarifa au tathmini inayofanywa baada ya utekelezaji wa jambo kufanyika kwa ajili ya uendelezaji au urekebishaji kulingana na utendaji ulivyofanyika  na mara nyingi hufanywa mwishoni mwa utekelezwaji. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
38.  Motisha/kichocheo (Motivation): Ni hali au kitendo kinachofanywa na mwalimu wakati wa kufundisha ili kuwafanya wanafunzi wapende na wavutike na somo kwa njia ya kuwapongeza, kuwasifu, kuwapazawadi nakadhalika. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
39.  Fikiri (think): Ni msamiati anaotumia mwalimu anapotaka kuwambia wanafunzi waweze kutoa/ kuelezea dhana ya jambo fulani. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
40.  Sikiliza (listen): Huu ni msamiati ambao hutumika pale mwalimu anapotaka asikilizwe wakati anapofunisha ili aweze kueleweka au kufahamika. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
41.  Jaribu (try): Msamiati huu unatumika pale mwalimu anapomtaka mwanafunzi aweze kusema au kuandika kitu/jambo kwa mujibu anavyoona au kuhisi kulingana na akili yake. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
42.  Kufahamu (to understand): Msamiati huu hutumika pale mwalimu pale mwalimu anapowauliza wanafunzi kama wamefahamu juu ya lile alilofundisha au wanafunzi wanapomuhakikishia mwalimu kama wameelewa juu ya lile walofundishwa. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
43.  Uchambuzi (analysis): Msamiati huu hutokezea pale wanafunzi endapo hawakufahamu katika jambo fulani na kutaka ufafanuzi zaidi kutoka kwa mwalimu. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
44.  Majadiliano (discussion): Ni mbinu ambayo hutumika pale mwalimu anapowataka wanafunzi waweze kujadili vipengele fulani katika mada anayoifundisha. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
45.  Jibu (answer): Ni mrejesho ambao hutumika pale mwalimu anapouliza suali na kutaka kupatiwa jibu kuhusiana na lile alilouliza. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
46.  Somo lililopita (previous lesson): Msamiati huu hutumika pale mwalimu anapotaka aunganishe mawazo ya wanafunzi kuhusu somo lake jipya kotokana na somo lililopita yaani kuwakumbusha wanafunzi kutokana na somo lililopita ili waweze kuelewa kwa urahisi somo jipya. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
47.  Soma (read): Msamiati huu hutumika pale mwalimu anapotoa kipande cha habari na kumtaka mwanafunzi aweze kusoma ili wenzake waweze kumsikiliza. Msamiati huu ni katika uga wa ufundishaji.
48.  Mtaala (curriculum): Ni hati/nyaraka maalumu inayotumika kuorodhesha yale yote yaliyopangwa kusomeshwa skuli yakiwa rasmi au sio rasmi. Msamiati huu ni katika uga wa Mitaala.
49.  Muhtasari (syllabus): Ni kifaa cha mtaala kinachotumika kuorodhesha mada zote zinazopaswa kufundishwa katika kila somo. Msamiati huu ni katika uga wa Mitaala.
50.  Kujisahihisha (self criticism): Ni msamiati unaotumiwa na mwalimu katika kumfanya mwanafunzi aweze kujirekebisha mwenyewe na kutoa maoni yake katika somo kama limefahamika au halikufahamika na hatua atakazozichukua kama mwanafunzi hajaweza kujirekabisha. Msamiati huu ni katika uga wa Mitaala.
Misamiati iliyotajwa hapo juu na ambayo hayakuainishwa katika uwanja wa Elimu na ufundishaji, kiujumla misamiati hiyo ni muhimu sana katika tendo zima la ufundishaji na ujifunzaji ambalo huwapelekea wadau wa elimu kama vile wakuza mitaala, watafiti, walimu na mwanafunzi kupata usahihi wa taarifa zinazotolewa.







MAREJEO.
Bukagile, G. & Masebo, J. B. (2008). Kiswahili kwa shule za sekondari: Kidato cha pili. Nyambari Nyangwine  publishers: Dar-es-salaam, Tanzania.
Coombs, B. (1995). Succeful Teaching: Apractical Hand book. Heinemann Educational books LTD: USA.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la pili. (2004).Oxford University Press: Kenya.
Katabaro, A . R. et al. (2003). Moduli ya somo la upimaji, tathmini na utafiti. Taasisi ya Elimu Tanzania: Dar-es-salaam, Tanzania
Ndalu, A.E. et al. (2014). Kamusi teule ya Kiswahili: kilele cha lugha. Toleo la kwanza. Printwell Industries Ltd: Kenya.
Youssef K.Y. (1998). Dictionary of the Terms of Education: Librairie du Liban Publishers: Beirut, Lebanon.
                                                                                                                 




Jumanne, 5 Julai 2016




UCHAWINI KUNA MAMBO
1.      Ukitaka ngia huko, wallahi utashituka
Utakutia vituko, vivyo navyo patashika
Utajutia kuwepo, na huruma kukushika
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

2.      Vizuu wa uchawini, kiwaona tashituka
Tadhani ni hayawani, hali imebadilika
Si kichwa si miguuni, sura zao kama paka
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

3.      Viongozi wa wachawi imeni imewatoka
Yao kwa hustawi, vizuu kupukutika
Ta siku moja haiwi, mmoja akasikika
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

4.   Uchawini ni hatari, ukatili meongoka
Kuna watu majabari, tena wasotikisika
Wamekuwa majeuri, kwa kile wanachotaka
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

5.      Ajira ya uchawini,  kama ya mkwe na kaka
Mavunoye huyaoni, ni viboko na kuchoka
Utaona kisirani, na akili kukuruka
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

6.      Ukichoka uchawini, kamwe usijeropoka
Watakuweka pembeni, na njaa itakufika
Ubakie masikini , iwe huna pa kushika
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

7.      Siku ukiwa na ombi, ndipo hapo utachoka
Waonekana cha zombi,  ulokosa pa kushika
Utakuwa cha mbirimbi, kwa kisu utakatika
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

8.      Mwisho naliweka tojo kuonesha nimefika
Uchawini si porojo, kila mtu akacheka
Utanywishwa ta mkojo, watu kimya kukuweka
Uchawini kuna mambo, si kama yalivyo huku

NA: SALEH ZAHRAN ABDULLA- CHAWAKAMA-SUZA